Siku chache baada ya Zoezi la kusikiliza kero za wananchi kimkoa kuzinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mh. CPA Amos Makalla, Mkuu wa Wilaya ya Magu Rachel Kassanda amesema hakuna kero ya mwananchi itakayoachwa kusikilizwa wilayani humo kwani wamejipanga kutembelea Kata na vijiji vyote kwaajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
DC Kassanda ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa zoezi la kusikiliza kero za wananchi Wilaya ya Magu katika ofisi za Halmashauri leo Jumatano Julai 20, 2023.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo DC Kassanda amesema kuwa Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaagiza kwaajili ya kufanya kazi hiyo na kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao hivyo ameahidi kuwa watafanya kazi hiyo kwa umakini mkubwa.
" Kuna baadhi ya wananchi wanatoka kata za mbali na hawana uwezo wa kuja hapa Halmashauri kuwasilisha kero zao hivyo uongozi wa Wilaya utakwenda katika Kata na Vijiji vyao kwaajili ya kusikiliza na kutatua kero zao" amesema DC Kassanda.
Ameongeza kuwa " Timu yangu ya wataalamu ikiongozwa na Kamati ya ulinzi na usalama , Mkurugenzi mtendaji, wakuu wa idara na taasisi zote za serikali zilizopo Wilaya ya Magu tutazunguka kila Kata ili kusikiliza na kutatua kero za wananchi "
Nao baadhi ya wananchi waliofika kuwasilisha kero zao katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Magu wameupongeza uongozi wa mkoa wa Mwanza kwa kuzindua zoezi hilo na kubainisha kuwa litasaidia kutatua kero za wananchi, kupunguza malalamiko na kuongeza ufanisi wa utendaji wa viongozi.
Zoezi la kusikiliza kero za wananchi kimkoa lilizinduliwa rasmi Septemba 18, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mh. CPA Amos Makalla na kuwaagiza viongozi kutoa ushauri wa kisheria mapema kwa wananchi ili kuepusha mashauri yao kufika mahakamani.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa