KATIBU Tawala Milaya ya Magu, Zuberi Said Zuberi amewataka waganga wa tiba asili wanaofanya shughuli zao katika wilaya hiyo kudumisha amani pamoja na kuzingatia wajibu wao wa kujisajili ili wapate vibali vitakavyowawezesha kutambulika kisheria.
Pia amewaomba kushirikiana na serikali katika mchakato mzima wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu ikiwa ni pamoja na kuhamasisha jamii kushiriki uchaguzi huo.
DAS Zuberi ametoa wito huo jana tarehe 15 Julai, 2025 mjini Magu katika mafunzo ya siku moja yaliyoshirikisha waganga zaidi ya 100 kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kushirikiana katika kutunza amani na kuepukana na ramli chonganishi.
“Ni haki ya msingi kufanya shughuli ya uganga, lakini haki ina wajibu, bila wajibu ni fujo… mtu kufanya shughuli hii bila kibali ni kwamba anakwenda tofauti na taratibu. Kwa sababu ninyi mnashughulikia na jamii moja kwa moja.
“Kuna takribani waganga 700 katika wilaya ya Magu, lakini waliojisajili ni 409, kwa hiyo kama mkihudumia watu watatu kwa mwezi ni sawa na watu 1,227 ambao mmewahudumia, ni wengi sana lakini mkitaka kutendewa haki mjue wajibu wetu kuzingatia taratibu,” amesema na kuongeza.
“Uchaguzi ni mchakato, ulianza muda mrefu ikiwemo kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, rai yetu kwenu ni kuwaomba kuhamasisha watu kushiriki uchaguzi, tuwe mabalozi wa kutoa hamasa kuhusu suala la ushiriki wa uchaguzi,” amesema.
Naye Mkuu wa Polisi Wilaya ya Magu - Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi SSP, Haji Makame aliwaonya waganga hao kuacha kutumia maabara za ramli chonganishi.
“Kufanya ramli ndio kunatuletea shida ndani ya wilaya yetu. Vitu vya msingi tunavyowataka ni kwamba mtoe taarifa kwa sababu haiwezekani mtu atoke Kenya au Tanga aje kufanya vitu vya ajabu Magu alafu ninyi mkae kimya, mkimtaja tukamdhibiti mapema na wilaya yetu itaendelea kuwa shwari. Tunajua wapo wanaokuja wanajificha kwenye vi-gesti nawahakikishia tunafuatilia tutawakamata mmoja mmoja,” amesema.
Mwenyekiti wa waganga wilaya ya Magu, Malale Mirambo aliahidi kusimamia utekeleza wa maagizo yote yaliyotolewa kwao na kuwataka waganga wenzake kwenda kujisimamia.
“Kila kata wajisimamie wenyewe, ambaye hataki kujiunga na umoja wetu kwa kukata kibali rasmi, ninawaomba polisi mkamateni mpelekeni ndani.
“Ninaagiza waganga wote waliopo ndani ya Magu, kama hauna kibali kuanzia jumatatu ijayo ahame kwenye wilaya ya Magu, kwa sababu lazima tutakukamata,” amesema.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa