Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Magu imetoa mafunzo elekezi kwa walimu 120 ajira mpya waliohudhuria mafunzo hayo ambapo walimu 57 ni wa shule za sekondari na 63 shule za msingi katika wilaya ya Magu.
Akifungua mafunzo hayo katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Magu zilizopo Ilungu wilaya humo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya hiyo, Mohamed Ramadhani amewataka walimu kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia nidhamu ya kazi.
Pia amewataka kutambua thamani ya wao kuwepo kwenye nafasi hizo kwamba wanamuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa majukumu yao hivyo wasiendekeze urasimu pindi watakapokuwa kwenye nafasi zozote za uongozi.
"Napenda mfahamu ya kwamba utumishi wa umma ndio injini ya Serikali lakini mtambue kuwa watumishi wote wa umma ni wawakilishi au wasaidizi wa Rais kwa maana hiyo mnatakiwa kuishi kwa nidhamu na uweledi hata katika jamii inayowazunguka vivyo hivyo kwenye utekelezaji wa majukumu yenu,” amesema.
Naye Katibu msaidizi TSC Wilaya ya Magu, Emanuela Chacha ametoa rai kwa walimu hao kubadili mtindo maisha kwa kuachana na mambo yasiyofaa na kuvaa uhusika wa mtumishi wa umma kwa kuwa na haiba nzuri wakati wote.
Akitoa mada ya katika mafunzo hayo, Afisa Utumishi wilaya ya Magu, Henry Sadatale amewataka walimu kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayosimamia utumishi wao wakati wote wa ajira.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa