MKUU wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Jubilate Win Lawuo ameongoza kikao cha maandalizi ya mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 kilichofanyika leo tarehe 10 Julai, 2025 katika ofisi za Halmashauri ya wilayani hiyo na kuwasisitiza waratibu kujipanga ili Magu iibuke kinara katika ukaguzi wa miradi na maandalizi ya mbio hizo.
Lawuo ameongoza kikao hicho kwa mara ya kwanza akiwa mkuu wa wilaya ikiwa ni wiki chache zimepita tangu Rais Samia Suluhu Hassan amteua kurithi mikoba ya Joshua Nassari. Awali Lawuo alikuwa Katibu Tawala wa wilaya hiyo.
Amesema Mwenge wa Uhuru katika awamu hii Magu itaupokea tarehe 27 Agosti katika uwanja wa Jiwe la Mkapa Kisesa kutoka wilaya ya Ilemela kisha kuukabidhi wilaya ya Kwimba.
Kikao hicho kimewakutanisha viongozi mbalimbali wa wilaya, akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Magu, Mohamed Ramadhani, viongozi wa vyama vya siasa, asasi za kiraia, watendaji wa kata, wakuu wa idara na wakuu wa taasisi za umma.
Wengine ni Waratibu wa Mwenge wa Uhuru ki-wilaya, Maafisa Uchaguzi, na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.
Mwenge wa Uhuru 2025 una kaulimbiu isemayo: “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu.”
Kaulimbiu hiyo inalenga kuhamasisha ushiriki mpana wa wananchi katika mchakato wa kidemokrasia, huku amani na utulivu vikitajwa kuwa nguzo muhimu za maendeleo ya taifa.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa