KATIKA kutekeleza kwa vitendo lengo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuinua sekta ya umwagiliaji kwa asilimia 50 ifikapo 2030, Mbunge wa Magu, Boniventura Kiswaga ametoa msaada wa pampu kwa wakulima wa kikundi cha Bustani kwa ajili ya kuboresha shughuli za kilimo cha umwagiliaji.
Kikundi hicho kilichopo katika Kijiji cha Kabale kata ya Jinjimili wilayani Magu mkoani Mwanza, kinaendesha shughuli za kilimo cha umwagiliaji kwa kuzalisha mazao ya nyanya na mahindi.
Akikabidhi msaada wa pampu hiyo yenye thamani ya Sh milioni 1.5 leo Jumamosi katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Magu – Ilungu kwa niaba ya Kiswaga, Diwani wa Kandawe, Lucas Bomoa (CCM) amewasisitiza wakulima hao kuitunza pampu hiyo na kuongeza uzalishaji wa mazao yao kama walivyomuomba mbunge huyo pindi alipowaahidi kuwasaidia.
Akipokea pampu hiyo kwa niaba ya wanakikundi wenzake ambao jumla wapo 10, Katibu wa Kikundi cha Bustani, Maduhu Manyilizo mbali na kumshukuru mbunge huyo kwa kutekeleza ahadi ya msaada huo wa kikundi, ameahidi kwenda kuongeza uzalishaji kutokana na urahisi wa umwagiliaji walioupata.
“Tuna jumla ya hekari tatu za kilimo cha umwagiliaji, lakini tulikuwa tunamudu kulima hekari mbili tu, sasa kwa msaada huu tutaweza kulima zote tatu na kuongeza mazao yetu ambayo ni nyanya na mahindi. Tunamshukuru sana mbunge wetu kwa msaada huu kwa sababu awali tulikuwa tunatumia ndoo kumwagilia ila sasa pampu hii itakuwa msaada mkubwa kwetu katika kukuza shughuli hizi za kilimo cha umwagiliaji,” amesema.
Katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020, Serikali iliboresha miundombinu ya umwagiliaji nchini, hivyo kuongeza eneo linalomwagiliwa kutoka hekta 461,000 mwaka 2015 had kufikia hekta 694,715 mwaka 2020.
Hata hivyo, Kwa mujibu wa Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 (The National Irrigation Master Plan) Tanzania ina eneo la hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji.
Kati ya hekta hizo, hekta milioni 2.3 zinauwezekano mkubwa wa kumwagiliwa, hekta milioni 4.8 zinauwezekano wa kati na hekta milioni 22.3 zina uwezekano mdogo wa kumwagiliwa.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa