Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Magu kwa kupata Hati inayoridhisha ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka mitatu mfululizo.
Pia ameitaka Menejimenti ya halmashauri hiyo kuja na mpango wa kufuta ufaulu wa daraja la nne na sifuri kwa wanafunzi ili kuhakikisha dhamira ya serikali ya kuboresha elimu inafikiwa kwa wanafunzi kupata daraja la kwanza.
Balandya ametoa maagizo hayo jana tarehe 17 Juni, 2025 wakati akiongoza baraza maalum la hoja za CAG kwa halmashauri hiyo kuishia Juni 30, 2024 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Said Mtanda.
Awali akiwasilisha taarifa ya ukaguzi mbele ya baraza hilo, Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Nje Mkoa wa Mwanza, Henry Chausa amebainisha kuwa 2023/24 halmashauri hiyo ilikaguliwa na kupata hati inayoridhisha na kwamba kuna hoja 46 ambazo zinafanyiwa kazi na kufungwa.
Baada ya kupokea taarifa hiyo Balandya amesisitiza hoja zote ambazo hazijatekelezwa ziwekewe mkakati wa utekelezaji wake ili zifungwe.
“Hivyo naagiza muweke vielelezo na viambatanisho vyote ndani ya muda ili kuifanya halmashauri ibaki salama,” amesisitiza Katibu Tawala.
Akizungumzia hoja kuhusu ufaulu kwa mwaka 2021-2023, katibu tawala huyo ameitaka menejimenti ya Magu kufuta kabisa daraja sifuri.
“Naomba tukajifunze kwenye halmashauri zingine wanafanyaje kuinua ufaulu mathalani Kwimba twendeni tuone wao wamewezaje kwani mazingira yetu hayatofautiani," amesema Balandya.
Ameongeza kuwa madiwani na watendaji ni wazazi na walezi hivyo wana wajibu wa kuwafundisha stadi za maisha watoto kama kufanya usafi wa mazingira na miili yao ili kuwafanya wawe na utayari na kujenga tabia ya kujitegemea.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Magu, Simon Mpandalume akichangia hoja hiyo, amefafanua kuwa tayari menejimenti ya halmashauri hiyo imeshafanikiwa kuongeza madarasa mapya, kujenga shule mpya ili kukabiliana na tatizo la utoro wa wanafunzi waliokuwa wanatembea umbali mrefu kufika shule.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa