ZAIDI ya Sh milioni 250 zilizotolewa na mfuko wa jimbo wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu kwa kipindi cha miaka mitano (2020-2025), zimetajwa kuchochea kasi ya maendeleo ya miradi mbalimbali ikiwemo ya afya, elimu, miundombinu na kuunga mkono juhudi za wananchi katika uibuaji wa miradi hiyo.
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu na Mbunge wa Magu, Boniventura Kiswaga katika kikao cha kuhitimisha ziara za kukagua miradi iliyotekelezwa na mfuko huo wa kuchochea maendeleo ya jimbo (CDFF).
Katika kikao hicho kilichofanyika kwenye ofisi za halmashauri ya Wilaya ya Magu zilizopo Ilungu, pia kilienda sambamba na kukabidhi kompyuta ya kisasa pamoja na kichapishi (printer) vilivyokabidhiwa kwa uongozi wa shule ya sekondari Kitumba.
Amesema fedha hizo zimeimarishaji ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwamo ujenzi wa shule za msingi, sekondari na zahanati na nyumba za watumishi.
“Kwa mwaka huu pekee tumesambaza Sh milioni 84 ambazo tumepokea kutoka serikali kuu na kuifanya jumla ya fedha za mfuko wa jimbo kwa miaka mitano kuwa Sh milioni 250 ambazo zimetumika kusambaza vifaa mbalimbali kama mabati kwa ajili ya kuezeka zahanati, shule za msingi, sekondari na nyumba za watumishi.
“Tumejitahidi kupeleka kwenye vitu vinavyoonekana kama inavyoelekezwa. Tumechangia vya kutosha kwa kuunga mkono pia juhudi za wananchi. Tumpongeze Rais Samia Suluhu Hassan kwani ameleta fedha nyingi kukamilisha uibuaji wa miradi hii ya wananchi huku halmashauri nayo ikichangia asilimia 40 kupitia mapato yake ya ndani,” amesema.
Akizungumza msaada huo wa kichapishi na kompyuta kwa shule ya sekondari Kitumba, Kiswaga amesema aliona vipaji vya wanafunzi katika moja ya mahafali aliyohudhuria shuleni hapo hivyo kuamua kuwaunga mkono wanafunzi hao ili kuendeleza vipaji vyao vya uchoraji.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Magu, Mohamed Ramadhani, Afisa Mipango wa wilaya ya Magu, Pastory Mukaruka amesema kupitia mfuko huo wa jimbo wamegawa vifaa mbalimbali vinavyokwenda kuchochea maendeleo kwenye jimbo hilo ikiwemo kuhamasisha wananchi waendelee kuchangia maendeleo yao.
Awali akizungumza kwa niaba ya wazazi, Mwenyekiti wa bodi wa shule ya sekondari Kitumba, Obedi Mwinula amemshukuru mbunge huyo pamoja na Rais kupitia halmashauri kwa namna anavyoboresha sekta ya elimu kwa ujumla.
Naye Mkuu wa shule sekondari Kitumba, Thomas Yakwala amesema vifaa walivyopatiwa vinakwenda kuleta chachu hasa ikizingatiwa mtaala ulioboreshwa unataka mwanafunzi ajifunze na kutoka shule akiwa na uwezo wa kujiajiri.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa