Mkuu wa Wilaya ya Magu Mh. Rachel Kassanda amezindua programu ya malezi , makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT MMMAM) katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu ikiwa na lengo la kukabiliana na kutokomeza changamoto zinazoonekana kuwa ni kikwazo cha hatua sahihi za ukuaji timilifu wa mtoto kimwili, kiakili na kijamii.
Akizungumza wakati akizindua programu hiyo leo Alhamisi Febuari 15 , 2024 DC Kassanda ametoa rai kwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu na idara zote zinazotekeleza program hii kwa kushirikiana na wadau kuzingatia utekelezaji Programu hii kwenye maeneo yao kupitia maelekezo na ushauri utakaokuwa na unaotolewa mara kwa mara.
Amesema Uzinduzi huu unafanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu ikiwa ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kuwa Programu hii izinduliwe ngazi zote kuanzia Taifa, Mkoa hadi Halmashauri.
"Uzinduzi huu uambatane na utekelezaji wake kwa kuweka Mipango Kazi na kusaidia utengaji wa bajeti na kutoa fedha kwa utekelezaji; amesema "
Kwa upande wake Afisa ustawi wa jamii Wilaya ya Magu, Coretha Sanga amesema kuwa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi, na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT MMMAM), inayotekelezwa kuanzia 2021/22 hadi 2025/26, inakusudia kuharakisha upatikanaji wa matokeo chanya ya maendeleo ya awali ya mtoto.
Ameongeza kuwa Programu za malezi jumuishi nchini Tanzania zinahitaji kupewa kipaumbele na msisitizo, kutokana na kukosekana kwa uratibu mzuri.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Bi. Fidelica Myovella amesema Halmashauri imejipanga kutekeleza programu hiyo kwa kushirikiana na wataalamu na wadau na kufanyia kazi maelekezo na ushauri uliotolewa na Mkuu wa Wilaya ili kufikia malengo ya utekelezaji wa programu hiyo.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa