Katika kuadhimisha siku ya mashujaa Jilai 25, 2024 viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Kamati ya Ulinzi na Usalama, viongozi wa dini, wameshiriki zoezi la usafi wa mazingira katika eneo la hospitali ya Wilaya ya Magu ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku hiyo ambayo huenzi na kukumbuka mazuri yaliyofanywa na mashujaa Tanzania.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo Katibu Tawala wa Wilaya ya Magu Jubilate win Lawuo ametoa wito kwa wananchi wa Magu kuendelea kuwaenzi mashujaa kwa kua wazalendo na kulinda amani ya nchi kwani ndo msingi wa maendeleo ya Taifa.
Amesema watanzania wote wanatakiwa kuienzi misingi imara ya kizalendo amani na upendo iliyojengwa na waasisi wa Taifa Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, misingi ambayo matunda yake tunayafaidi watanzania wote na tujipange kurithisha na vizazi vijavyo.
"Tumekuja hapa kwaajili ya kumbukumbu ya wazalendo wetu waliojitoa kipindi hicho katika kulipigania Taifa letu na matunda yake tunayaona hadi leo na vizazi vyetu vutakuja kufaidi matunda haya" amesema DAS Lawuo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mohamed Ramadhani amesema Magu inawakumbuka mashujaa kwa kujitoa kwao na kusababisha Taifa kupata ukombozi ambao hadi leo watanzania wanaendelea kufaidi matunda yaliyotokana na ukombozi huo.
Aidha amesema kuwa mbali na kuwakumbuka Mashujaa waliopigania Uhuru pia usafi huo umekua ni sehemu ya kuwakumbusha Wananchi kutunza mazingira ya Wilaya kwaajili ya afya ya Jamii huku akiwahimiza kufanya usafi kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku na sio kusubiri matukio maalumu.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa Dini Shekh wa Kata ya Isandula Majaliwa Rashid akiwakilisha Shekh Mkuu wa Wilaya amesema viongozi wa dini wataendelea kuwakumbuka mashujaa kwa kuwaombea dua kwa mazuri waliyofanya na kusema kuwa wataendelea kuliombea Taifa liendelee kuwa na amani na mshikamano.
Kila ifikiapo Julai 25 ya kila Mwaka,Tanzania huadhimisha siku ya kuwakumbuka Mashujaa waliopoteza Maisha yao wakiutetea,Kuupigania na Kulinda Uhuru wa Tanzania. Kwa upande wa Wilaya ya Magu Siku hii pia imeambatana na Shughuli mbalimbali ikiwemo dua na sala maalumu za kuwaombea Mashujaa waliopoteza maisha na kuiombea Amani ya Nchi kutoka kwa Viongozi wa Dini na kushiriki zoezi la usafi katika hospitali ya Wilaya .
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa