Magu, Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Magu Mh. Joshua Nassari amefanya ziara ya ukaguzi katika mradi wa jengo la ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Magu ambao unatekelezwa na Mkandarasi wa Suma JKT ambapo hadi sasa jengo limefikia hatua ya ukamilishaji kwa kufanya skiming, kuweka vigae, kufunga mfumo wa maji, umeme na vioo.
Akizungumza wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo leo Jumatano Aprili 03, 2024 DC Nassari amesema Mkandarasi aongeze spidi ili ujenzi ukamilike mapema na kwa wakati.
Amesema kukamilika kwa ujenzi huo utasaidia kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi wa Magu pamoja na usimamizi wa watumishi wanapokua katika majukumu yao ya kazi.
Aidha DC Nassari amesisitiza kuzingatia suala la ulinzi na usalama wa vifaa vya ujenzi wa jengo hilo ili vitumike kama ilivyokusudiwa na kukamilisha ujenzi wa jengo bila upotevu wa vifaa ambao unaweza kuongeza gharama za ziada .
Katika ziara hiyo Dc Nassari aliambata na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Ramadhani, baadhi ya Wakuu wa idara na kamati ya ulinzi na usalama.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa