Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA) kinatarajia kuwanoa wanawake zaidi ya 1000 wilayani Magu kuhusu masuala mbalimbali ya ukatili wa kijinsia na namna ya kujua haki zao katika umiliki wa ardhi kisheria.
Pia kinatarajia kuwezesha mchakato uanzishwaji wa sheria ndogo za kijiji zenye mrengo wa kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Hayo yamebainishwa na Mwanasheria kutoka Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Wakili Lightness Raimos alipokutana na wakuu wa idara wa halmashauri ya wilaya ya Magu kwa lengo kuutambulisha mradi Mwanamke Dhabiti katika ngazi ya halmashauri.
Amesema kupitia mradi huo wa Mwanamke Dhabiti, TAWLA wanalenga kumaliza aina zote za ukatili wa kijinsia na kuhakikisha wanawake wanajua haki zao katika kumiliki mali.
“Mradi ulianza rasmi toka Aprili mwaka huu kwa ajili ya utekelezaji lakini ni mradi wa miaka mitatu. Ni mradi ambao utatumia njia mbalimbali kuhakikisha malengo yake yanafikiwa kwa kutoa msaada wa kisheria kwa makundi yote hususani wanawake na wasichana.
“Tutatoa elimu mbalimbali za kisheria, tutasaidia wanawake waliopo kwenye vikundi kupata na kumilikishwa ardhi kisheria, tutawezesha mchakato mzima wa uwepo wa sheria ndogo za kijiji zenye mrengo wa kijinsia,” amesema.
Aidha, amesema wameleta pendekezo linalohusu moja ya mikakati ya utekelezaji juu ya sheria ndogo ili waweze kushirikiani na vijiji ambavyo vimetajwa kufanikisha zoezi zima la utungaji pamoja na upitishaji wa sheria ndogo ya kijiji.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa